Askofu wa jimbo katoliki la Isiolo Anthony Ireri Mukobo amewarai wananchi kufanya maamuzi mwafaka kuhusu viongozi kwa kutathmin sera na wala si kwa kushurutishwa kuwaunga mkono baadhi ya viongozi.
Akiongea wakati wa ibada ya misa ya jumapili katika kanisa la Mtakatifu Eusebio mjini Isiolo, askofu Ireri alisema kwamba wakenya wana haki ya kujiamulia kiongozi anayewafaa kulingana na sera zake atakazowauzia.
Baadhi ya wanasiasa wanaokusudia kuwania viti kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 wamekuwa wakipata uungwaji mkono kutoka kwa viongozi wa jamii, huku wengine wakipendekezwa na wakuu serikalini.
“Tunaomba viongozi watuongoze kwa njia ya amani na kwa kufuata katiba ya nchi. Na kipindi hiki tunapoelekea uchaguzi mkuu, tuchague viongozi kulingana na sera na vilevile uwezo wa mtu kupeana huduma hitajika kwa wananchi. Wakenya wanajua kujichagulia bila kushurutishwa, bila kuambiwa lazima umchague huyu ama yule.”
Askofu Ireri vilevile alisisitiza ujumbe wa baraza la maaskofu wa kanisa katoliki KCCB kwa serikali kuhusu chanjo ya Covid-19, akisema kuwa serikali haifai kuwalazimisha wananchi kupokea Chanjo hiyo.
Kwenye barua waliotuma kwa vyombo vya habari na asasi za serikali baada ya kongamano lao kila mwaka, maaskofu wa kanisa katoliki waliishauri serikali kwamba chanjo ingefaa kuwa uamuzi wa mtu binafsi, wala si kwa kushurutishwa.
Askofu Ireri hiyo jana alisisitiza ujumbe huo wa KCCB, “Tuendelee kujikinga na Covid-19. Virusi vina uwezo wa kubadilikabadilika kila mara kwa hivyo tuendelee kufuata maagizo ya serikali kwa kuvaa barakoa na kuweka umbali. Hata hivyo serikali haifai kulazimishia watu chanjo. Huu ni uamuzi wa mtu binafsi.”
Wakati uo huo, askofu Ireri alihimiza haja ya viongozi kuchochea Amani na kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata haki.