Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu na waziri Charles Mugane Njonjo ameaga dunia.
Kifo chake kilitangazwa jumapili asubuhi na Rais Uhuru Kenyatta, ambaye alisema kifo cha Njonjo ni pigo kubwa kwa nchi, huku akituma salamu za rambi rambi kwa familia yake.
“Kwa niaba ya taifa la Kenya, familia yangu na kwa niaba yangu binafsi, natuma salamu za rambirambi kwa familia, marafiki na jamaa wa Njonjo, na Wakenya wote,” Uhuru Alisema
Mwendazake alipelekwa katika makafani ya Lee Funeral Home kwa matayarisho ya heshima za mwisho. Kisha baadae, Familia yake ilielekea Kariokor Hindu Crematorium ambapo mwili wa mwendazake ulichomwa.

Njonjo ndiye mjumbe pekee aliyesalia hai katika Baraza la Mawaziri wa wakati wa baada ya kupigania uhuru wa Kenya. Rais Kenyatta alisema Kenya ina deni la shukrani kwa Njonjo na viongozi wa kizazi chake cha enzi ya uhuru kwa mchango wao wa kujitolea katika kuweka msingi imara.
Njonjo aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa kwanza wa nchi baada ya uhuru kati ya 1963 na 1979, na Waziri wa Mambo ya Katiba kati ya 1980 na 1983.
Aliaga dunia saa kumi na moja asubuhi, ya Jumapili, Januari 2, 2022. Njonjo amefariki akiwa na umri wa miaka 101.