Staff Mail

CATHOLIC DIOCESE OF ISIOLO COMMUNICATION DEPARTMENT

HOFU YA VIRUSI KUENDELEA KUSHUHUDIWA NCHINI

Huku madhara ya virusi vya corona yakizidi kubadilisha shughuli za kila humu nchini baadhi ya makanisa na misikiti imetangaza kusitisha ibada pamoja na shughuli nyinginezo ili kuwakinga waumini kutokana na maambukizi ya virusi hivyo. Wa hivi karibuni ni Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Jackson Ole Sapit, ambaye ametangaza kusitishwa kwa huduma zote za kanisa ikiwemo ibada za Jumapili, sherehe za harusi na mazishi. Kwenye taarifa yake, Askofu Sapit amewataka waumini wote kuomba wakiwa nyumbani na familia zao na kuhakikisha kwamba wanajitenga na makundi ya idadi kubwa ya watu. Kuhusu sakramenti takatifu, askofu Sapit amesema shughuli hiyo itafanywa kwa utaratibu spesheli utakaotolewa. Waumini wametakiwa kushiriki ibada na maombi kupitia njia ya teknolojia. Ibada zitapeperushwa moja kwa moja kwenye mitandao kama vile Facebook na tovuti rasmi za kanisa hilo. Aidha amesema kwamba kila Jumapili kutakuwa na matangazo ya moja kwa moja kuanzia saa mbili asubuhi na Jumatano saa kumi na mbili jioni. Kanisa hilo pia limeitaka serikali kuongeza juhudi za kukabiliana na janga hili kwa kuhakikisha wafanyakazi wote wanalindwa na waajiri wao. Hapo jana msikiti wa Jamia ulitangaza kusitisha shughuli zake na ibada zote kwa waumini wake. Katibu mkuu wa kamati ya msikiti huo Abdul Bary Hamid alisema kwenye taarifa kuwa hakutakuwa na mikutano yoyote ya maombi katika msikiti wa Jamia kwa muda usiojulikana. Bw Hamid alisema uamuzi huo uliafikiwa baada ya mashauriano na baraza la Majlis Ulamaa na lile la wataalumu waislamu katika masuala ya matibabu (KAMMP).